MABINGWA watetezi, Yanga SC wameendeleza mwendo wa kusuasua katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya jioni ya leo kulazimishwa sare ya 0-0 na Mtibwa Sugar ya Morogoro Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
Sare hiyo inaifanya Yanga ifikishe pointi tisa baada ya kucheza mechi tano, ikishinda mbili na kutoa sare tatu, wakati Mtibwa inafikisha pointi 11 baada ya sare hiyo ya pili, ikiwa pia imeshinda mechi tatu.
Sifa zimuendee kipa wa zamani wa zamani wa Yanga, Benedicto Tinocco aliyesimama langoni mwa Mtibwa Sugar leo na kuikatalia kabisa timu yake ya zamani leo katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga, aliyesaidiwa na Robert Ruhemeja wa Mwanza na Abdallah Shaka wa Tabora.
Mchezo ulianza kwa kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu, ingawa Yanga ndiyo waliokuwa kulitia majaribu lango Mtibwa Sugar dakika ya tatu baada ya beki wake wa kushoto, Gardiel Michael kukimbia na mpira hadi kwenye boksi la timu ya Morogoro kabla ya kuangushwa, ingawa refa hakutoa penalti.
Mtibwa Sugar wakajibu dakika ya 12 baada ya kiungo wake, Hassan Dilunga kukaribia kufunga kama si beki wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ kuondosha mpira kwenye hatari.
Mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma akaikosesha Yanga bao dakika ya 14 baada ya kushindwa kumalizia pasi nzuri ya Mzambia, Obrey Chirwa na dakika ya 15 kipa Benedict Tinocco alidaka shuti kali la mshambuliaji Ibrahim Hajib kutoka nje kidogo ya boksi.
Hajib akapiga shuti zuri la mpira wa adhabu dakika ya 27 kutoka umbali wa mita 20, lakini kwa mara nyingine Tinoco, kipa wa zamani wa Yanga akaokoa.
Mtibwa Sugar wakajibu dakika ya 31 baada ya mshambuliaji mwenye umbo kubwa, Stahmili Mbonde kukosa nao la wazi kufuatia krosi nzuri ya Salum Kihimbwa.
Kipindi cha pili, Yanga waliendelea kulitia misukosuko lango la Mtibwa Sugar na dakika ya 51, shuti la kiungo Pius Buswita lilikwenda nje kidogo baada ya kusogea na mpira kutoka eneo la katikati ya uwanja.
Kiungo Mohammed Issa ‘Banka’ wa Mtibwa Sugar alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 63 baada ya kumchezea rafu beki wa Yanga, Gardiel Michael Mbaga na dakika ya 64 Ngoma tena akaikosesha timu yake bao baada ya kupiga kichwa lakini mpira ukadunda na kutoka nje.
Kipa Mcameroon wa Yanga, Youthe Rostand aliokoa mara mbili mfululizo mashuti ya mshambuliaji chipukizi wa Mtibwa Sugar, Kelvin Kongwe Sabato dakika ya 65 kwanza akitema na mpira kumrudia mchezaji huyo aliyepiga tena na mlinda mlango huyo akawahi kuinuka na kuokoa tena.
Gardiel Michael alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 69 baada ya kushika mpira akidhani umetoka.
Winga Geoffrey Mwashiuya alitia krosi nzuri langoni mwa Mtibwa Sugar dakika ya 74 na kumkuta Hajib aliyeunganisha nyavuni, Tinocco akaokoa ukamkuta Ngoma aliyepiga tena, lakini kipa wa Mtibwa akaokoa tena na mpira kumkuta Pius Buswita aliyepiga tena mpira ukaenda nje.
Dakika ya 89 kiungo wa Yanga, Said Juma 'Makapu' alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu kiungo wa Mtibwa Sugar, Mohammed Issa.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa: Youthe Rostand, Juma Abdul, Gardiel Michael, Andrew Vincent, Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’, Pius Buswita, Raphael Daudi/Geoffrey Mwashiuya dk71, Donald Ngoma/Juma Mahadhi dk77, Obrey Chirwa/Thabani Kamusoko dk56 na Ibrahim Hajib.
Mtibwa Sugar: Benedict Tinocco, Salum Kupela, Issa Rashid, Dickson Daud, Cassin Ponera, Shaaban Nditi, Salum Kihimbwa/Henry Joseph dk82, Mohammed Issa, Stahmili Mbonde/Ismail Aidan dk89, Hassan Dilunga/Kevin Sabato dk49 na Ally Makarani.
Comments
Post a Comment