Haya ndio Matukio yaliyotikisa soka 2017



LEO tumeuanza mwaka mpya wa 2018. Mwaka 2017 umemalizika  kukiwa na baadhi ya matukio yaliyotikisa na ya kukumbukwa kwa  upande wa soka la Kibongo.

Mwandishi wa makala haya amekusanya matukio matano  yaliyotikisa zaidi anga la michezo nchini Tanzania ambayo yalikuwa  kwenye vinywa, akili na kufuatiliwa na mashabiki wengi wa michezo  nchini.

SportPesa kuzidhamini Simba, Yanga, SingidaKampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa iliufanya mwaka 2017 kuwa wa neema baada ya kuzidhamini klabu kongwe nchini za  Simba, Yanga, lakini pia Singida United.

Mkataba wa klabu ya Simba uliingiwa Mei ukiwa ni wa miaka mitano, lakini mwezi huo huo, ilifanya hivyo kwa Yanga, kama vile haitoshi, Singida United nayo ikalamba udhamini mnono pia.

Ujio Klabu ya Everton BongoKampuni hiyo hiyo ya SportPesa Julai, iliileta klabu kubwa nchini  England ya Everton, ikiongozwa na mchezaji maarufu duniani Wayne  Rooney.

Timu hiyo iliweka kambi yake nchini kabla ya Ligi Kuu ya England  inayoendelea kuanza, lakini pia ilicheza mechi moja dhidi ya Gor Mahia  kwenye Uwanja wa Taifa.

Gor Mahia ilipata nafasi hiyo baada ya kuwa bingwa wa michuano  iliyoanzishwa na kampuni hiyo.

Usajili Niyonzima, AjibuTukio lingine lililoshtua na kusumbua vichwa vya mashabiki wa  soka nchini ni usajili wa wachezaji maarufu nchini, Haruna  Niyonzima na Ibrahim Ajibu.

Mpaka Juni mwaka huu, Niyonzima alikuwa Yanga na Ajibu alikuwa mcheza wa Simba.

Zilianza kama tetesi zozote zile za usajili duniani. Zilichukuliwa  kama hivyo, lakini kila siku zilivyozidi kusonga mbele hali ilikuwa  ikibadilika.

Zikawa si tetesi tena baada ya baadhi ya matukio  kuashiria kuwa wachezaji hao huenda wangehama kwenye klabu  zao. Wapo waliokuwa hawataki kuamini hilo. Waliona ni kama ndoto hivi.

Lakini Julai, Ajibu akatangazwa rasmi kuwa mchezaji wa  Yanga, huku Agosti, Niyonzima alithibitishwa rasmi kuwa ni mchezaji wa Simba.

Rumande Viongozi Simba, TFF

Moja ya matukio yaliyotikisa mwaka jana ni kukamatwa kwa  viongozi wa klabu ya Simba, Rais wake Evance Aveva na Makamu, Geofrey Nyange 'Kaburu' na kuswekwa mahabusu.

Lakini pia ni kukamatwa kwa na Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamal Malinzi na Katibu Mkuu wake, Selestine Mwesigwa.

Matukio haya yote yalitokea mwishoni mwa mwezi Juni.

Viongozi hao wote walikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na kushikiliwa kwa muda  kabla ya kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  na hadi leo hii, kesi zao bado zinaendelea na bado wako rumande  kutokana na kwamba kesi hizo hazina dhamana.

Makaso yanayowakabili kwa ujumla hayatofautiana sana kwani wanakabiliwa na tuhuma za kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo na  kutakatisha fedha.

Uongozi Mpya TFF

Katikati ya Agosti walipatikana viongozi wapya wa Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Katika uchaguzi ambao awali ulitawaliwa na kila aina ya mizengewe na vituko wakati mchakato huo unaanza, hatimaye Mwenyekiti wa Kamati uchaguzi mkuu wa TFF Revocatus Kuuli akamtangaza Wallace Karia kuwa Rais wa TFF.

Uchaguzi huo uliofanyika mjini Dodoma, Karia aliyekuwa Makamu  wa Rais, alimrithi aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini, Malinzi.

Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa TFF zamani wakati huo ikiitwa FAT, Michael Wambura, alichaguliwa kuwa  Makamu wa Rais.

Mabadiliko Uendeshwaji Simba

Baada ya mchakato wa muda mrefu, ulioanza mapema mwaka jana hatimaye mwanzoni mwa mwezi uliopita kazi hiyo ilikamilika na hatimaye mwanachama wa muda mrefu, Mohamed "MO" Dewji kushinda tenda ya kumiliki asilimia 49 ambapo klabu hiyo sasa itakuwa ikiendeshwa kwa mfumo wa hisa kutoka ule wa zamani wa kadi.Wanachama watamiliki hisa asilimia 50, kama ambavyo serikali ilivyoagiza.

Usajili wa Asante KwasiKwenye soka la Tanzania, imezoeleka kuwa kila muda wa usajili ni lazima kuwe na wachezaji ambao watakuwa gumzo.

Hata kama si wengi basi hata mmoja tu. Anaweza kuwa gumzo  kutokana na kugombewa na klabu kongwe za Simba na Yanga, au  wakati mwingine utata kwenye usajili wake.

Kwenye kipindi cha dirisha dogo Ligi Kuu msimu huu, hakukuwa na mbwembwe nyingi, zaidi ya utata wa usajili wa beki Mghana, Asante Kwasi.

Beki huyo mwenye nguvu na anayejituma alizua mzozo kwa timu za Simba na Lipuli. Wakati ikidaiwa kuwa amesajiliwa na Simba,  Lipuli ilidai kuwa ina mkataba naye na hawezi kwenda kokote.

Hii ilimfanya beki huyo kupamba kurasa za mbele za magazeti  ya michezo na vipindi vya michezo habari zilizovutia wasikilizaji  wengi zilikuwa za mchezaji huyo. Hata hivyo mambo yalimalizika kwa Simba kukubali kulipa Sh. milioni 25.

Maajabu Z'bar Heroes ChalenjiKingine kilichoshangaza na kushtua wengi ni kufanya vema kwa  Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Chalenji iliyofanyika  nchini Kenya.

Ikiwa ni timu ambayo haikutiliwa maanani, Zanzibar ilitolewa kwa  mbinde hatua ya fainali na wenyeji Kenya kwa mikwaju 3-2 ya  penalti. Hii ni baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 baada ya dakika 120.

Ikichukuliwa kama timu kibonde, Zanzibar iliichapa Tanzania Bara  kwenye hatua ya makundi mabao 2-1, kabla ya kuishindilia Rwanda  mabao 3-1.

Hapo ndipo kila mpenzi wa soka, alipoanza kuigeuzia macho, huku  viongozi wa CECAFA wakiwa hawaamini wanachokiona kutokana  na soka lao safi la kuvutia na kujituma.

Comments