Yanga kuchuana na Mbao FC leo


Picha ya mtandao

IKIWAKOSA nyota wake watano muhimu kwenye kikosi cha kwanza, Yanga itajitupa uwanjani leo Jumapili kuikabili Mbao FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

Mechi hiyo ni muhimu kwa Yanga ambayo itataka kurudisha heshima yake baada ya kufungwa mara mbili katika msimu uliopita huku ikitoka sare mchezo mmoja. Miwili ilikuwa ligi na mmoja Kombe la FA.

Timu hizo, zinavaana katika Uwanja wa CCM Kirumba huku Yanga ikimkosa Kelvin Yondani, Thabani Kamusoko na Donald Ngoma wenye majeraha, Ibrahim Ajibu mwenye kadi tatu za njano na Obrey Chirwa ambaye alisusa akaenda kwao Zambia.

Lakini Yanga ambayo itakuwa chini ya Kocha Msaidizi, Shadrack Nsajigwa kutokana na George Lwandamina kufiwa na mwanae, italazimika kutumia masha-mbulizi ya kushtukiza pamoja na kuweka ukuta mzito kutokana aina ya wachezaji ilionao.

Hiyo, ni kutokana pia na uimara wa kikosi cha Mbao kinachou-ndwa wachezaji wengi chipukizi wenye kasi wanao-cheza soka la pasi nyingi huku wakisha-mbulia kwa wakati mmoja.

Katika mazoezi ya mwisho, Nsajigwa alionekana akiwaandaa mabeki wa pembeni Juma Abdul akicheza namba mbili na Hassan Kessy ambaye ataanza kama ilivyo kwa Pius Buswita ambaye atatumika kama kiraka.

Wakati akiibadilisha safu ya ulinzi ya kulia, kocha huyo alionekana akimuandaa Gadiel Michael kucheza namba tatu huku Haji Mwinyi akipangwa namba kumi na moja akichukua nafasi ya Emmnauel Martin na lengo la kocha huyo kuona wachezaji wake wakicheza kwa kushambulia na kulinda goli lao ndani ya dakika 90 mchezo ili kuwapunguza kasi Mbao.

Wakati akiimarisha safu ya pembeni, katikati napo huenda kukawepo mabadiliko ambako beki mkongwe, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliondolewa na kumpisha Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye ni kijana mwenye kasi atakayeweza kuendana na kasi ya wachezaji hao vijana wa Mbao.

Safu ya kiungo wa kati, Papy Kabamba Tshishimbi ambaye tegemeo aliyerejea hivi karibuni akitoka kwenye majeraha ya enka yeye ataanza kucheza namba sita huku Raphael Daudi akicheza nane.

Na Buswita yeye ataingia kucheza namba kumi ambayo ametolewa na Kessy katika namba saba ambayo anaicheza tangu ajiunge na Yanga akitokea Mbao katika msimu huu na Yohana Nkomola atacheza namba tisa baada ya Mrundi, Amissi Tambwe kujitonesha goti lake mechi iliyopita ya Kombe la FA dhidi ya Reha FC iliyomalizika kwa Yanga kushinda mabao 2-0 kati ya hayo moja likifungwa yeye.

Akizungumzia mechi hiyo, Nsajigwa alisema kuwa “Malengo yetu ni kuchukua pointi muhimu zitakazotuweka katika nafasi nzuri katika msimamo wa ligi,ninaamini mechi itakuwa ngumu katika pande zote kwani kila timu imejiandaa, tutaingia uwanjani tukiwa na kisasi cha kufungwa mara mbili .
BEKI MBAO

Yusuph Ndikumana raia wa Burundi amekipiga mkwara kikosi cha Yanga; “Dakika 90 ndizo zitaamua nani ataibuka mshindi. Nimejipanga kuhakikisha naisaidia timu yangu, kuimarisha ukuta wetu ili kutowapa nafasi wapinzani kutufunga.”

BUSWITA

Kiungo wa zamani wa Mbao FC ambaye kwa sasa yupo Yanga, Pius Buswita alifichua kwamba; “Wachezaji wenzangu wa zamani wa Mbao FC walinipigia simu na kuniambia kwamba watanionyesha kazi tutakapokutana kwani ni lazima wanizuie nisiweze kufanya chochote kama ambavyo nimekuwa nikifanya katika mechi zilizopita.

“Lakini kwangu nimejipanga vilivyo kuhakikisha kwamba nafanya makubwa katika mchezo huu na kuwapelekea kilio ambapo nimepanga lazima nifunge ila sitaweza kushangilia kwa sababu wao ndiyo walionifanya niweze kutambulika,” alisema Buswita.

KOCHA MBAO

Kocha wa Mbao FC, Ettiene Ndairayije alisema ; “Tumejipanga vizuri na hatuna hofu yeyote na Yanga kwani tumejiandaa vya kutosha kupata ushindi katika mchezo huo na hawana wasiwasi juu ya hilo kwani Yanga hawana historia ya kutufunga.”

Comments