Aliyezaa na Masogange aeleza mapya




SIKU moja baada ya mazishi ya aliyekuwa mwigizaji wa filamu na video queen maarufu Bongo, Agness Gerald Waya ‘Masogange’ yaliyofanyika juzi, jioni, kijijini kwao, Utengule-Usongwe wilayani Mbalizi jijini Mbeya, mwanaume aliyezaa naye, Sabri Shaban, kwa mara ya kwanza amezungumza na Risasi Mchanganyiko na kuelezea mapya kuhusu maisha yake na staa huyo.

MTOTO MIAKA 11
Kabla ya msiba huo, Sabri aliyezaa na Masogange mtoto mmoja wa kike aitwaye Sanie Sabri mwenye umri wa miaka 11, hakuwa akifahamika kwa watu wengi. Pia watu wengi walikuwa wakishindwa kujua kama Masogange ana mtoto au la.

WASHIRIKIANA MALEZI
Katika mahojiano maalum na gazeti hili, baada ya msiba huo mzito, Sabri alisema kuwa, kifo cha Masogange kimeacha pengo kubwa mno katika maisha yake kwani walikuwa wakishirikiana katika malezi ya binti yao huyo ambaye kwa sasa yupo darasa la saba.

KILA MMOJA NA MAISHA YAKE LAKINI…
Alisema kwamba, licha ya kuwa alikuwa yeye na Masogange hawakuwa pamoja kwa miaka mingi iliyopita huku kila mtu akiwa na maisha yake baada ya kumzaa mtoto huyo, bado walikuwa wanampa malezi mazuri mtoto huyo kwani kuna wakati alikuwa akiondoka kwa baba yake (Sabri), Magomeni na kwenda kuishi kwa mama yake (Masogange), Makongo- Juu jijini Dar kisha kurejea tena kwa baba yake.

“Ni pigo kubwa sana kwangu na kwa mwanangu Sanie. Alikuwa ametuzoea mimi na mama yake. Tulikuwa tunamlea mtoto wetu pamoja. Hata yeye (Sanie) alifurahia sana uwepo wa mama yake.

AENDA KUMPUMZISHA MZAZI MWENZAKE
“Sasa tunaongea hapa, mama yake hayupo tena. Kwa kweli Agness (Masogange) ameniachia pengo kubwa sana maishani mwangu, ninamuomba Mungu ampe nguvu mwanangu (Sanie) katika kipindi hiki kigumu,” alisema Sabri ambaye alisafiri na msiba hadi Utengule, Mbalizi jijini Mbeya kushuhudia mzazi mwenzake akipumzishwa kwenye nyumba yake ya milele.

SANIE KUSOMESHWA HADI CHUO KIKUU
Wakati mzazi huyo akifunguka hayo juu ya mtoto wao huyo, mmiliki wa Shule ya St. Patrick ya jijini Dar, Ndele Mwaselela, yeye alijitolea kumsomesha Sanie hadi elimu ya chuo kikuu endapo atafanikiwa kufaulu katika masomo yake.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa Aprili 23, 2018 na Kamati ya Maandalizi ya Mazishi iliyoandaliwa na Bongo Movies kwenye Viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar, Sanie ni mtoto wa pekee wa Masogange na Sabri.

Kamati hiyo kupitia mwekahazina wake, Zamaradi Mketema ilieleza kuwa, ilimwekea shilingi milioni 2 zilizobaki katika michango ya msiba huo kwenye akaunti yake. Zamaradi alisema kuwa, kiasi hicho cha fedha kitasaidia kuwa kianzio cha ada atakapoanza kidato cha kwanza mwakani kwa kuwa mwaka huu anatarajiwa kumaliza darasa la saba.

KUTOKA LEADERS HADI UTENGULE
Masogange alipatwa na umauti Ijumaa iliyopita katika Hospitali ya Mama Ngoma iliyopo Mwenge jijini Dar alipokuwa amelazwa kwa takriban siku nne ambapo taarifa za awali zilieleza kuwa, mrembo huyo amefariki dunia kwa ugonjwa Pneunomia na tatizo la upungufu wa damu mwilini.

Mara baada ya kuagwa katika Viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar, Jumapili iliyopita, mwili wa Masogange ulisafirishwa kwenda kupumzishwa katika makazi yake ya milele, juzi, Jumatatu iliyopita kijijini kwao, Utengule wilayani Mbalizi jijini Mbeya

Comments