BEKI wa pembeni wa Mtibwa Sugar, Nickson Kibabage amesaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Kibabage aliyekuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kilichoshiriki fainali za Afrika Mei mwaka huu nchini Gabon, anasimamiwa na akademi ya Cambianso ya Dar es Salaam.
Alijiunga na kikosi cha pili cha Mtibwa Sugar msimu uliopita na baada ya uzoefu mkubwa alioupata akiwa na Serengeti Boys, sasa ameanza kukomazwa kikosi cha kwanza.
Nickson Kibabage (kulia) amesaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro. Kushoto ni Mratibu wa Mtibwa, Jamal Bayser
Katika hatua nyingine, kipa Abdallah Makangana ambaye yuko nje ya uwanja kwa takribani wiki moja sasa akiendelea na matibabu kutokana maumivu aliyoyapata akiwa anafanya mazoezi, anaendelea vizuri.
“Ninaendelea vizuri, ni jambo la kumshukuru Mungu kadiri siku zinavyokwenda mbele na hali yangu ya kiafya inazidi kuimarika na ninataraji kupewa ruhusa hivi karibuni ya kujiunga na wenzangu kuendelea harakati za kupigania timu,”amesema.
Msimu huu, Abdallah Makangana ametumikia Mtibwa katika michezo mine tu kabla ya kuumia kufanya idadi ya majeruhi kufikia wane, wengine ni wakiwa ni kipa Shaaban Hassan Kado, beki wa pembeni Salum Kupela Kanoni na kiungo Henry Joseph Shindika.
Wachezaji wa Mtibwa Sugar wamepewa likizo ya wiki moja kufuatia Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kusimama kwa wiki mbili hadi tatu kupisha michuano ya CECAFA Challenge inayoanza Desemba 3 nchini Kenya.
Comments
Post a Comment