Ngorongoro. Hifadhi ya Ngorongoro inatarajiwa kunufaika zaidi baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kuiweka katika mchakato wa orodha ya maeneo ya kimataifa ya kipekee yanayojumuisha uhifadhi na maendeleo endelevu ya jamii (Unesco Global Geoparks).
Hatua hiyo itaiwezesha hifadhi hiyo kuingia katika orodha ya dunia ya kijiolojia itakayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, hivyo kuaminiwa kimataifa na kuwezesha kutembelewa na watu wengi wakiwemo watalii.
Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro, Dk Freddy Manongi amesema hati ya usajili wa kupandishwa hadhi inatarajiwa kutolewa na Unesco hivi karibuni baada ya kukamilika kwa mchakato.
Dk Manongi amesema Hifadhi ya Ngorongoro kwa sasa ipo katika orodha ya Unesco ya maeneo ya urithi wa dunia. Eneo hilo la kijiolojia linaruhusiwa kuishi wanyamapori na kuendeleza mila za watu wa makabila ya Masai, Hadzabe na Barbaig.
Hifadhi hiyo iliyoko katika bonde la ufa la Mashariki lilipata hadhi ya kimataifa ya kuwa katika orodha ya maeneo ya urithi wa dunia mwaka 1979.
Hifadhi ya Ngorongoro ndilo eneo ambalo limeendeshwa kwa mafanikio kwa mtindo wa kuchanganya matumizi ya binadamu (wafugaji) na uhifadhi. Watu 88,000 wanaishi katika eneo hilo kwa amani na utulivu na wanyamapori.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kujitangaza kimataifa na kuaminiwa zaidi, hivyo kunufaika na idadi kubwa ya wageni watakaotembelea Hifadhi ya Ngorongoro.
Mkazi ndani ya hifadhi hiyo, John ole Kuyan amesema mchakato huo wa Unesco ni faraja kwao kwa sababu wametambuliwa kuwa ni sehemu ya Ngorongoro.
“Tutahakikisha tunahuisha utamaduni wa Kimasai, Kihadzabe na Kibarbaig kwa sababu ni asili ambayo kama tukiipuuza inaweza kupotea kama ambavyo tamaduni nyingine zilivyosahaulika,” amesema Ole Kuyan.
Comments
Post a Comment