Hii ndio ripoti ya idadi ya Watu Tanzania



Ripoti ya makadirio ya watu nchini inaonyesha Tanzania kuna idadi ya watu 54.2 milioni hadi kufikia mwaka 2018 huku ikieleza kuwa kila mwaka kuna ongezeko la watu milioni 1.6.

Ripoti hiyo inaonyesha Tanzania Bara ina watu 52.6 na Zanzibar milioni 1.6  inaifanya Tanzania kuwa nchi ya sita barani Afrika kwa ongezeko kubwa la watu ikitanguliwa na Nigeria, Ethiopia, DRC na Misri.

Akizindua ripoti hiyo leo Jumatano Februari 28, 2018 Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango amesema idadi hiyo ya watu inakadiriwa kufikia 77.5 milioni ifikapo mwaka 2030 wakati nchi zote duniani zitakuwa zinatathmini mafanikio na changamoto za Malengo ya Mpango wa Dunia wa Maendeleo Endelevu (SDGs).

Amesema kwa kuzingatia matokeo ya sensa ya watu ya mwaka 2012, inakadiriwa kuwa kila mwaka kuna ongezeko la wastani wa watu wapatao 1.6 milioni hapa nchini.

"Ongezeko hili linatokana na idadi kubwa ya vizazi vipatavyo milioni 2 ikilinganishwa na idadi ndogo ya vifo ambavyo nintakribani 400,000 kwa mwaka," amesema.

Kutokana na takwimu hizo, Dk Mpango amesema hairuhusiwi shirika lolote kufanya makadirio ya idadi ya watu na kuchapisha makadirio hayo bila kuishirikisha Ofisi ya Taifa ya Takimu (NBS).

"Kwa kufanya hivyo ni kosa, makadirio hayo hayaendani na hali halisi ya watu na inahatarisha maendeleo ya nchi. Takwimu za nchi ambazo vigezo vyake haviendani na hali halisi vinapotosha hali ya ustawi wa nchi na wananchi waje," amesema.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa amesema kasi hiyo kubwa ya ongezeko la watu inasababishwa na kiwango cha juu cha uzazi  ambapo tafiti zinaonyesha wastani wa mwanamke kuzaa ni watoto watano kwa kipindi chake cha uzazi.

Amesema pia kasi hiyo inasababishwa na matumizi madogo ya njia za uzazi, umaskini na kiwango duni cha elimu miongoni mwa wanawake hasa katika maeneo ya vijijini.

Comments