Majeraha ya Neymar yamchefua Zidane



Zinedine Zidane

Kocha wa Klabu ya Real Madrid, Zinedine Zidane amefunguka kuhusu majeraha yanayomkabili mshambuliaji wa Paris St. Germain, Neymar Jr kwa kusema kuwa amechukizwa kwani alitaka awepo kwenye mchezo wa marudiano wa Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA Champions) wiki lijalo.

Zidane amesema kuwa kuumia kwake kunafanya kuwe na utofauti kwenye mchezo huo kwani Neymar ni mchezaji mwenye kipaji na uwezo mkubwa uwanjani.

“Kuumia kwake sio pigo la PSG ni pigo kwa watu wote wapenzi wa soka duniani, ningependa kumuona anacheza kwani najua mchezo ungekuwa wa tofauti sana,“amesema Zidane jana usiku kwenye mkutano wake na Waandishi wa Habari baada ya mchezo wa Real Madrid na Espanyol kumalizika.

Neymar aliumia kwenye kifundo cha mguu wikiendi iliyopita kwenye mchezo kati ya PSG dhidi ya Marseille ambapo kwa ripoti rasmi iliyotolewa na Baba yake mzazi ambaye ndiye wakala wake amesema uwezekano wa kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya Madrid bado ni mdogo.

Soma zaidi – Neymar hati hati kukosa mchezo dhidi ya Madrid, Barcelona wapatwa na pigo

Aidha, Zidane alizungumzia kuhusu mbio za Real Madrid kutetea ubingwa wa La Liga, ambapo amesema kuwa mbio hizo bado ni ndefu ingawaje kimtazamo watahitaji kushinda mechi zote huku wakitegemea matokeo ya michezo mingine.

“Ligi bado ni ngumu ukiangalia ushindani wa juu ni dhahiri safari bado ni ndefu, tutajitahidi kushinda kila mchezo ili kuweka matumaini ingawaje bado tutahitaji matokeo ya michezo mingine, nadhani lolote linaweza likatoa lakini bado sio kazi rahisi,“amesema Zidane.

Jana usiku klabu ya Real Madrid imekubali kipigo cha goli 1-0 dhidi ya Espanyol na kuwafanya kusalia nafasi ya tatu ya msimamo wa La Liga, ambapo wanakuwa chini ya alama 14 kutoka kwa vinara wanaoongoza kwenye msimamo Barcelona.

Comments