Arsenal watupwa nje Europa League



 Kocha wa Arsenal Arsene Wenger alipoteza fursa pekee ya kushinda kombe msimu wake wa mwisho akiwa katika klabu hiyo baada ya kuchapwa na Atletico Madrid katika nusu fainali ya ligi ndogo ya klabu Ulaya Europa League.

Arsenal walishindwa kwa jumla ya mabao 2-1.

Mechi ya mkondo wa kwanza, matokeo yalikuwa 1-1 lakini kwenye mechi ya Alhamisi iliyochezewa Madrid, mshambuliaji wa zamani wa Chelsea Diego Costa alirejea kuwaadhibu Gunners alipofunga bao dakika za mwisho mwisho za kipindi cha pili (dakika ya 45+2).

Kwa bao hilo, Costa alifuta matumaini ya Arsneal ya kushinda kombe msimu huu na kucheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.

Bao la Costa lilitokana na pasi muhimu kutoka kwa mshambuliaji Mfaransa Antoine Griezmann ambaye amekuwa akitafutwa na klabu kadha kuu Ulaya.

Ulikuwa usiku usio wa bahati kwa Arsenal kwani nahodha wao Laurent Koscielny aliondolewa uwanjani kwa machela baada ya kuumia kwenye kano za sehemu ya nyuma ya kifundo cha mguu.

Comments